Isaiah 59:4-8


4 aHakuna hata mmoja anayedai kwa haki;
hakuna hata mmoja anayetetea shauri lake kwa haki.
Wanategemea mabishano matupu na kusema uongo,
huchukua mimba ya magomvi na kuzaa uovu.

5 bHuangua mayai ya nyoka wenye sumu kali
na kutanda wavu wa buibui.
Yeyote alaye mayai yao atakufa,
na wakati moja lianguliwapo, nyoka hutoka humo.

6 cUtando wao wa buibui haufai kwa nguo;
hawawezi kujifunika kwa kile walichokitengeneza.
Matendo yao ni matendo maovu,
vitendo vya jeuri vipo mikononi mwao.

7 dMiguu yao hukimbilia kwenye dhambi,
ni myepesi kumwaga damu isiyo na hatia.
Mawazo yao ni mawazo maovu;
uharibifu na maangamizi huonekana katika njia zao.

8 eHawajui njia ya amani,
hakuna haki katika mapito yao.
Wameyageuza kuwa njia za upotovu,
hakuna apitaye njia hizo atakayeifahamu amani.

Copyright information for SwhKC